Dereva bodaboda wa Mji Mdogo wa Qatesh wilayani Hanang’ Mkoa wa Manyara, amekatwa sikio kwa kisu kwa tuhuma za kufumaniwa akiwa na mke wa dereva wa teksi. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi, Francis Massawe alisema tukio hilo lilitokea Desemba 21 saa 6:10 usiku kwenye Kitongoji cha Qendangonyi, Kata ya Ganana wilayani Hanang’. Kamanda Massawe alisema chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi na majeruhi amepata kilema cha maisha baada ya sikio kutolewa. Alisema wanamshikilia dereva teksi kwa uchunguzi wa tukio hilo kabla ya kumfikisha mahakamani.