By
Unknown
Baada ya ugonjwa wa mafua ya ndege kugundulika nchi jirani ya Uganda baada ya kuwepo kwa vifo vingi vya ndege pori katika maeneo ya Lutembe beach, Masaka, Kachanga, Bukibanga na Bukakata na vifo hivyo kutokea kwa baadhi ya ndege wafugwao (kuku na bata) na inahisiwa kuwa ndege hao wamepata virusi vya ugonjwa huo kutoka kwa ndege pori wanaohama kutoka nchi za Ulaya.
Baada ya taarifa hizo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto leo January 18 2017 imetoa taarifa kuhusu kuwepo kwa virusi vya mafua makali ya ndege katika nchi jirani ya Uganda. Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa maeneo yalioathirika ni maeneo yanayozunguka ziwa Victoria pamoja na ziwa lenyewe.
Taarifa iliyotolewa na wizara ya afya imesema kuwa hadi sasa hakuna binadamu yeyote aliyeonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo huko nchini Uganda hivyo wametoa tahadhari kuwa kuna uwezekano mkubwa wa ugonjwa kusambaa kwa binadamu ikiwa hatua madhubuti za kujikinga hazitazingatiwa.
Taarifa ya wizara imetaja haya ya kuzingatia ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo
- Kutoa taarifa endapo wataona kutokea kwa vifo vya ndege pori au wafugwao (kuku, bata na wengineo) kwa wataalamu wa mifugo, afya au ofisi ya serikali iliyo karibu nawe
- Kutokugusa mizoga au ndege wagonjwa bila kutumia vifaa kinga
- Kuepukana na tabia ya kuishi nyumba moja na ndege wafugwao
- Kuepuka kuchinja kuku au bata wanaoonyesha dalili yoyote ya ugonjwa
- Kunawa mikono vizuri kwa kutumia sabuni
- Kupika nyama au mayai ya ndege kwa muda mrefu usiopungua nusu saa. .
- Kuepuka kushika ndege wa porini na ndege wa majumbani wanaohisiwa kuwa na ugonjwa huu.
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment